Tuesday, March 30, 2010

Mchungaji Kipala wa Wikipedia ya Kiswahili

Ingo Koll au Kipala ni mhariri ambaye ametunga makala mengi yenye kilobaiti nyingi kuliko mwandishi yeyote wa Wikipedia ya Kiswahili. Makala zake nyingi zinahusu masula ya kijamii, dini, siasa, na maisha ya kila siku ya binadamu. Kwa namna moja au nyingine, aliandika makala ya Vita Kuu ya Dunia ya Kwanza na ya Pili, Vita Baridi, Mkataba wa Versailles, Jumuiya ya Madola, Bahari ya Shamu, Mfumo_wa_jua_na_sayari_zake, na nyingine nyingi tu! Kipala, ni mchangia aliyechangia kwa muda mrefu sana bila kusimama. Inawezekana akawa mchangiaji pekee mwenye idadi kubwa ya makala kuliko wachangiaji wengine. Kipala, ndiye mwongozo wa Bwana Muddyb (mwenye nyumba hii), ambaye alitiwa moyo wa kuendelea kuchangia Wikipedia ya Kiswahili - kwani yeye ni Mswahili na anastahili kukuza lugha yake kupitia mitandao kama ile. Basi niseme pongezi kwake kwa kila jambo aliloniambia. Tena amenifunza mengi sana katika Wikipedia ile. Niseme tu, hongera zake hizoooooooo!! Bila kusahau huyu bwana ni mchungaji wa Kilutheri. Hivyo, busara zimeja, na kwake ndipo pa kuzipata! Salam teeeele zikufikie!

Shukrani,Muddyb

Kutana na Oliver Stegen au Baba Tabita

Je, unajua kama kuna Mzungu anajua lugha za kienyeji za Tanzania? Lugha hizo ni pamoja na Kilangi na nyingine kadhaa za mkoni Dodoma. Mzungu huyo, hufanya shughuli za ushauri a kiisimu katika Afrika ya Mashariki. Lakini je ni nani huyo? Si mwingine, bali Oliver Stegen au Baba Tabita (pichani). Mwana-isimu huyo, anaishi mjini Nairobi na mara kwa mara tunakuwa nae kule katika Wikipedia ya Kiswahili. Kwa kweli, anatusaidia kuboresha istilahi zetu kwa kiasi kikubwa sana. Hivyo, tunamshukuru kwa kila namna. Michango yake Wikipedia ni kuhakikisha kwamba lugha sanifu inatumika katika Wikipedia ile na hata katika mitandao mingine inayohusiana na lugha Kiswahili. Tumaini lake hasa ni kuona Kiswahili kinatumika katika nyanja muhimu mbalimbali. Katika Wikipedia, husisitiza sana matumizi ya kutobadili neno kwenda neno. Yaani, ni lazima tuwe na mwelekeo mmoja na si mara hivi mara vile. Huo ndiyo mchango wake wa kiisimu katika Wikipedia yetu. Ametunga makala nyingi sana zinazohusiana na masuala ya Tuzo ya Nobel. Kwa namna moja au nyingine, aliandika makala za fasihi, kemia, elimu, historia na kadhalika. Kwa sasa, amesimama kwa muda, lakini tunategemea kurudi kwake mtandaoni hivi karibuni. Wasalam,

Muddyb

Monday, March 29, 2010

Martin Benjamin wa Kamusi Hai Mtandaoni

Kwenye Wikipedia ya Kiswahili kuna Wazungu wengi wanaochangia makala mbalimbali, lakini kuna mmoja ambaye ameijitoa siku nyingi ili kuendeleza suala la ujanibishaji wa lugha ya Kiswahili mtandaoni. Mtu huyo, ni Martin Benjamin wa Kamusi Hai Mtandaoni. Zamani, alikuwa kama mwalimu katika chuo kikuu cha Yale, huko nchini Marekani. Akiwa chuoni, alifundisha masuala ya sayansi ya jamii na Kiswahili. Katika Wikipedia, alitumia jina la Malangali kwa sababu aliwahi kuishi mjini Malangali, Iringa. Tangu 2007, ameanza kazi za ujanibishaji mapaka sasa. Kazi ni pamoja na kubadilisha kusano za Wikipedia ya Kiswahili, na kazi nzima ya uchakataji na kuendeleza Kamusi Hai. Pia, hushughulikia lugha za Kiafrika. Kifupi, ni mwanaharakati wa kweli. Hasa katika kuendeleza Kiswahili mtandaoni. Pongezi kwake, na ni matumaini yangu kumuona akiendelea kufanya shughuli za kuendeleza Kiswahili mtandaoni. Kila la heri kwake Martin.Ahsante,
Muddyb


Saturday, March 27, 2010

Wazungu wa Wikipedia ya Kiswahili

Hivi una habari kwamba Wikipedia ya Kiswahili ilipiga hatua kubwa baada ya idadi ya Wazungu kuongezeka? Aliyeanzisha Wikipedia ya Kiswahili ni Mjerumani mmoja mwenye jina la Marcos Cramer mnamo mwaka wa 2003. Hebu soma historia fupi alioiandikia mwenyewe kwa lugha ya Kiswahili (usishangae ukikuta makosa madogomadogo - anajua Kiswahili kiwango cha kati tu):


"Mwezi wa 12 mwaka 2003 niliangalia Wikipedia ya Kiswahili. Nikatambua kwamba yaliyomo hayakuwa habari za kamusi elezo. Kwa kweli kulikuwa na "makala" mbili au tatu tu, zilizokuwa na habari kutoka tovuti nyingine; aidha kulikuwa na "makala" chache zilizokuwa na tafsiri ya Kiingereza ya neno moja tu. Mwanzoni nilihariri bila kuingia. Kwa hiyo ni kigumu kupata hariri zangu za kwanza. Anuani za IP nilizozitumia kwa uhakika zilikuwa anuani zinazoanza na "163.1.209" na zinazokamili na ".239" hadi ".245". Hariri ya zamani zaidi ambayo ninajua kwamba ni yangu ni uundaji wa makala Kiesperanto tarehe 7 mwezi wa 12 mwaka 2003. Tarehe 5 mwezi wa pili mwaka 2004 nilianza kufanya kazi nyingi zaidi: Kwanza niliunda makala tatu Lugha iliyotengenezwa, Lugha asilia na Lugha saada ya kimataifa, baadaye nikaweka uelezaji wa kwanza kuhusu Wikipedia kwenye Ukarasa wa Mwanzo:
"Wikipedia ni mradi wa lugha nyingi wa kutengeneza kamusi elezo kamili na sahihi ya maandishi huru. Ilianzishwa kwa Kiingereza mwezi wa kwanza mwaka 2001, na mwaka 2003 imeanzishwa kamusi hii kwa Kiswahili. Kusema kwamba ni ''maandishi huru'' maana yake ni kwamba kila mtu anaweza kuikuza na kuibadilisha, hata usipofahamu mambo ya kompyuta. Uweke "Edit this page" tu, halafu badilisha au ongeza maandiko."
Msemo "kamusi elezo" niliubuni mwenyewe. Siku zile Kamusi Project ilikuwa na tafsiri "kamusi" tu kwa "encyclopedia", na kamusi yangu ya Kijerumani-Kiswahili haikuwa na tafsiri kwa "Enzyklopädie". Nilitaka kuzuia ukorogo kati ya kamusi (yaani kitabu chenye tafsiri za maneno) na kamusi elezo (yaani kitabu chenye maelezo kuhusu mambo mbalimbali; ukorogo huu tayari ilisababisha kwamba kulikuwa na makala zenye tafsiri za maneno kwa Kiingereza tu), kwa hiyo nilibuni msemo "kamusi elezo".
Tarehe 19 mwezi wa pilli nilihariri kwa mara ya kwanza kwa kutumia akaunti yangu: Nilibuni makala Hisabati na nilifanya makala Hesabu iwe na habari za kielezo. Baadaye nilijaribu kung'amua jinsi ya kutafsiri kusano (yaani "interface") kwa Kiswahili. Tarehe 31 mwezi wa 5 mwaka 2004 tayari nilikuwa mkabidhi na niliweza kutafsiri ujumbe za mfumo. Mwezi wa sita mwaka 2004 niliendelea kubuni makala au kufanya makala ziwe na habari za kielezo, kwa mfano Historia, Jumuia na Uislamu. Mwezi wa kwanza mwaka 2005 Neno (ambaye pia ni Mwesperanto) alishirikiana na Wikipedia ya Kiswahili (hasa alitafsiri ujumbe za mfumo), mwezi wa tisa mwaka 2005 Ndesanjo akaja, na mwezi wa 12 mwaka 2005 Kipala. Tangu mwisho wa mwaka 2005 mradi unaweza kuitwa mradi wenye uhai. Mpaka Muddy alishirikiana mwezi wa 8 mwaka 2007 wageni (yaani watu wasioongea Kiswahili kama lugha ya mama) walifanya sehemu kubwa ya kazi. Bado sasa karibu nusu ya hariri zinatoka kwa wageni.""


Basi huyo ndiye bwana Marcos! Haikushia hapo, kwa msaada wa Matt Crypto, Ndesanjo (Mswahili kutoka Tanzania), ChriKo, Kipala, Oliver Stegen au Baba Tabita (mwana-isimu pekee anayepatikana katika Wikipedia ya Kiswahili) waliendesha Wikipedia na kuweza kuanzisha makala za msingi za kamusi elezo na baadaye Kipala na Muddyb tukaanzisha mpya yenye kufuata mwelekeo wa kisasa zaidi!

Sasa tazama Wazungu hawa jinsi walivyo-hariri hadi sasa katika Wikipedia ya Kiswahili. Orodha hizo ni pamoja na:

Oliver Stegen au Baba Tabita mara: 23,086

Kipala mara: 16,322

Marcos mara: 406

ChriKo mara: 2,649

Matty Crypto mara: 931

Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa! Mpaka sasa, tumebaki na michango kadhaa tu kutoka kwa Wazungu hao. Mwanzoni mwa mwaka wa 2008, tukampata mchangiaji mwenye jina la Riccardo Riccioni, yeye huandika hasa masuala ya kidini. Ukizungumzia mambo hayo, basi mtapatana! Bila kusahau naye ni Mzungu kutoka nchini Italia, lakini anaishi Tanzania mpaka sasa. Kipala, shughuli za kimaisha zimembana kiasi kwamba hana tena muda mwingi kama awali. Oliver au BT, yu-mapumzikoni kiimani na hata kazi pia huchangia uadimu wake katika mtandao. ChriKo, ni mtu wa kusafiri nchi za kimagharibi, basi hata uwepo wake huwa wa mauzauza. Matt Crypto, kakimbia jumla tangu 2007 baada ya kumpa usimamizi mkuu Oliver - ndiyo ikawa basi. Marcos naye, ndiyo kama Matt tu. Saaana hupatika katika Wikipedia ya Kiensparanto! Jamani si tuwape pongezi Wazungu hawa? Basi pongezi kwao!!! Pia kuna Wazungu wengine ambao mara nyingi wao hutoa vitu vya msingi - sana hutoa taarifa za maendeleo ya mtandao wa Kiswahili katika ulimwengu wa Kiwiki-wiki. Wazungu hao ni pamoja GerardM, Guaka, Lloffiwr, Mr. Accountable, Jhendin, na wengine wengi tu kutoka nchi za Kimagharibi.

Mkutano wa Wikimania - 2010

Kama jinsi ilivyo-ada. Kila mwaka kuna kuwa na mikutano ya Wanawikipedia wote wanakutana kujadili nini kifanyike baada ya mwaka kwisha. Mjadala mkubwa hasa ni uendelezi na upanuzi wa mradi wa Wikimedia Foundation na watoto zake, yaani, Wikipedia, Wikichuo, Wikamusi, Wikispishi, Wikihabari, Wikidondoo, na kadhalika. Wikimania humanishaa kwamba "Wiki na zana za Kiwiki, yaani, mfumo tunaotumia au Wikitext za kiwiki kwa ajili uchangizi wa makala na habari nyinginezo". Halafu "MANIA" kutoka Kiingereza: Kupenda sana kitu - kwa maana hiyo hawa wote wanaoshiriki katika mkutano huu ni wapenda Wiki ndiyo sababu wanaita Wikimania! Taarifa ni kwamba mwaka huu mutano unafanyika mjini Gdańsk, Poland. Mikutano ya awali ilifanyika hapa: Buenos Aires, Argentina (2009) Alexandria, Egypt 2008) Taipei, Republic of China on Taiwan (2007) Cambridge, Massachusetts (2006) Frankfurt, Germany (2005) . Basi tangu ufanyika mkutano wa kwanza huko mjini Franfurt Ujerumani, kumekuwa na mfululizo wa mikutano hiyo kila mwaka. Tena kila mwenye kubahatika kuchaguliwa kwenda mkutanoni hupewa nafasi hiyo. Tangu mwaka wa jana, kumekuwa na kupewa kipaumbele kwa Waafrika kwenda huko kwa sababu waliowengi katika Afrika hawana uwezo wa kwenda nchi za mabali kama hizo. Hivyo, Wikimedia Foundation hutoa udhamini wa wachangiaji wake kwenda kushiriki katika mkutano. Basi kuwa mmoja wao!